Wakulima wa pamba wilayani Serengeti wahofia mfumo mpya wa ulipaji wa pamba wakidai kuwa mfumo wa zamani ni bora zaidi.
Hayo yamesemwa kupitia viongozi wa vyama vikuu na vya msingi katika kikao kazi kilichofanyika jana Mei 28 2018 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Wakitoa michango yao kwa nyakati tofauti Bwana Madaraka Gesura kutoka kikundi cha Nganyani A kilichopo katika Kijiji cha Wagete Kata ya Rigicha alisema kuwa wakulima wengi wa pamba wapo vijijini hivyo ni vyema wakilipwa huko huko kuliko kulipwa fedha zao kupitia akaunti za benki, huduma ambayo hutumia umbali mrefu kuifikia. Naye Bwana Julius Wanduku kutoka kikundi cha Nguvu moja kilichopo katika Kijiji cha Mosongo Kata ya Mosongo anasema kuwa mfumo mpya wa ulipaji ni kero kwa wakulima wadogo wa pamba ambao hupokea kiasi kidogo cha fedha ambayo ikipitia katika taasisi za fedha hukatwa, hivyo ni vyema wakulima wakilipwa pesa zao mkononi.
Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti, Bwana Cosmas Quamara akifafanua jambo katika kikao kazi na Vyama vya Ushirika vya Pamba wilayani Serengeti.
Akitoa ufafanuzi wa hoja hizo za wakulima, Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti Bwana Cosmas Quamara alisema kuwa Serikali imetoa mwongozo wa shughuli yote ya ukusanyaji na uuzaji wa pamba kutoka kwa wakulima, hivyo ni vyema wakazingatia maagizo yaliyotolewa na Serikali. Aidha kuhusu malipo ya fedha kupitia taasisi za fedha Bwana Quamara alisema kuwa ni vyema wakulima wakilipwa kupitia akaunti zao za benki huku akisema kuwa ni njia yenye usalama zaidi kwa fedha za wakulima
“Hapo nyuma tumekuwa tukiona wakulima wakidhulumiwa au kuibiwa fedha za mazao waliyouza, hivyo kupitia benki wakulima wanakuwa na usalama zaidi na fedha zao kwakuwa malipo yataingizwa moja kwa moja kwenye akaunti zao.” Alisema Bwana Quamara na kuendelea kwa kusema kuwa kuweka akiba katika taasisi za fedha kunapungua matumizi yasiyo na ulazima huku akiwasisitiza viongozi wa vyama hivyo kuongeza hamasa ili wakulima wengi wafungue akaunti katika taasisi za fedha huduma ambayo hutolewa bila gharama yoyote.
Katika kikao hicho vyama vikuu na vya msingi vilikabidhiwa mizani, vibao vya gredi ya pamba, stakabadhi na hati za malipo ili kufanikisha kazi ya ukusanyaji na uuzaji wa pamba.
Msimu wa ununuzi wa pamba wilayani Serengeti unatarajiwa kufunguliwa mapema mwezi Juni mwaka huu (2018) huku bei ya pamba ikitarajiwa kuwa ni Shilingi 1100 kwa kilo moja ya pamba ya gredi A na Shilingi 600 kwa kilo moja ya pamba ya gredi B.
MATUKIO KATIKA PICHA
Viongozi wa Vyama vya ushirikia vya Pamba wilayani Serengeti wakisikiliza jambo kwenye kikao.
Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Bi. Eliza Simon akitoa maelekezo ya uendeshaji wa zoezi la ukusanyaji wa pamba kwa Viongozi wa Vyama vya ushirika wilayani Serengeti
Mkaguzi wa Pamba kutoka Bodi ya Pamba Bwana Shabani Ramadhani akitoa maelekezo ya namna ya kutumia mizani kwa ajili ya upimaji wa pamba.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti