Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri leo Septemba 13, 2025 amefanya ziara Wilayani Serengeti ambapo katika ziara hiyo ametembelea Mradi wa Maji wa Miji 28 unaotekelezwa katika eneo la Bwawa la Manchira na kujionea shughuli mbalimbali zinazoendelea katika mradi huo na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili uweze kakamikika kwa muda uliopangwa.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo Eng. Mwajuma amesema azma ya Serikali ni kutatua kero ya maji katika maeneo yote nchini hivyo kukamilika kwa mradi huo kutaondoa changamoto ya maji katika Mji wa Serengeti hivyo akamtaka mkandarasi kuongeza nguvu kazi katika utekelezaji wa mradi huo ili ifikapo mwezi Desemba wananchi wa Serengeti waweze kupata maji ya uhakika.
"Kukamilika kwa mradi huu hapa Serengeti kutaondoa kabisa changamoto ya maji kwa wakazi wa mji wa Serengeti na maeneo ya jirani. Hivyo basi, hakikisheni mradi huu unakamilika kwa wakati kwa kuongeza nguvu kazi na vifaa ili Desemba mwaka huu wananchi waanze kunufaika na maji ya uhakika," amesema Mhandisi Mwajuma.
Mradi wa Maji wa Miji 28 katika mji wa Mugumu - Serengeti unaotekelezwa na Mkandarasi Mega Engineering and Infrastructure Company Limited kutoka nchini India unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 21 unatarajia kukamilika Mwezi Desemba 2025 ambapo kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuondoka adha ya maji kwa wakazi zaidi ya Laki moja wa Mji wa Serengeti na viunga vyake.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti