Wilaya ya Serengeti ilianzishwa mwaka 1974 baada ya kugawanywa kutoka Wilaya ya Musoma huku Mugumu ikifanywa kuwa makao makuu ya Wilaya.
Mhe. A. Nyemela aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya wa kwanza na Bw. B. Salim aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya wa kwanza. Wilaya hii ilipoanzishwa ilikuwa na tarafa 4 za Rogoro, Serengeti, Nansimo na Kenkombyo pamoja na Majimbo mawili ya Uchaguzi ya Serengeti na Nyamuswa.
Mwaka 1978 ilianzishwa Wilaya ya Bunda, Kata ya Ngoreme ambayo ilikuwa sehemu ya Wilaya ya Musoma ikawa tarafa ya Ngoreme katika Wilaya ya Serengeti huku Kata za Nansimo na Kenkombyo zikaunda Wilaya ya Bunda, hivyo Wilaya ya Serengeti ikabaki na tarafa 2 za Rongoro na Ngoreme. Kwa sasa Wilaya ya Serengeti ina Tarafa 4, Kata 30 na vijiji 78, Vitongoji 363 na Kaya 41,570.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi, mwaka 1978 Wilaya ya Serengeti ilikuwa na watu 207,688 ikijumuisha wakazi wa Wilaya ya Bunda kabla haijaundwa. Sensa zilizofuata zilionyesha kuwa mwaka 1988 ilikuwa na watu 111,710, mwaka 2002 ilikuwa na watu 176,609, mwanaume 84,263 na wanawake 92,346.
Sensa ya mwaka 2012 Wilaya ilikuwa na Wakazi 249,420 kati yao wanaume ni 121,399 (48.68%) na wanawake ni 128,021 (51.33%)
Kwa kutumia makadirio ya sense ya watu na makazi ya mwaka 201, mwaka 2016 Wilaya ya Serengeti ilikadiriwa kuwa na watu 275,223 kati yao wanaume ni 133,958 na wanawake 141,265
Jiografia na Hali ya Hewa ya Wilaya
Wilaya ya Serengeti ina ukubwa wa km² 10,373 iko kati ya Nyuzi 10° 30’Kusini 20° 40’Kusini mwa Ekweta nyuzi 34° 15’ Mashariki 35° 15’ Mashariki mwa Greenwich Meridian. Kati ya eneo hilo kilometa za mraba 7,000 ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Serengeti National Park). Aidha kilometa za mraba 189.63 ni eneo la “Ikorongo Game Reserve”. Kilometa za mraba 66.39 ni eneo la “Grumeti Game Reserve”, na kilometa za mraba 245.6 ni eneo la wazi (open area). Eneo lililobaki la kilometa za mraba 659 ni eneo la kilimo, ufugaji na makazi ya watu.
Wilaya hupata wastani wa mvua kati ya Milimita 600-1200. Mvua hunyesha mara mbili kwa mwaka kati ya miezi ya Agosti-Desemba na Februari hadi April. Ukanda wa juu hupata wastani wa mm 1200, ukanda wa kati wastani wa mm 1000-1200 na uwanda wa chini mm 600 -1000. Wastani wa joto nyuzi 26 °C wakati wa kiangazi.
Mji wa Mugumu Serengeti
Hifadhi ya Taifa ya Mbuga ya Serengeti
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti