MUSOMA – Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi, ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mara na wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Mto Mara (Mara Day) yanayotarajiwa kufanyika kuanzia kesho Septemba 12 hadi Septemba 15 mwaka huu katika Viwanja vya Mwenge Wilayani Butiama.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Septemba 11, 2025 Mhe. Mtambi amesisitiza kuwa, lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha umma juu ya umuhimu wa kuhifadhi vyanzo vya maji na ikolojia ya Mto Mara na kuongeza kuwa mto huo ni rasilimali muhimu si tu kwa Mkoa wa Mara na Tanzania, bali pia kwa mamilioni ya viumbe hai wakiwemo wanyama wanaohama kila mwaka kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti hadi Maasai Mara nchini Kenya huku akisisitiza kuwa uhai wa bonde hilo unaenda sambamba na uhai wa jamii na uchumi wa nchi.
Aidha, Mhe. Mtambi ametoa rai kwa wakazi wa Wilaya zote za Mkoa wa Mara zinazozunguka bonde la mto Mara na zile zisizopakana na mto huo, kujitokeza kwa wingi na kuunga mkono juhudi za serikali katika kulinda mazingira.
Maadhimisho ya mwaka huu yanatarajiwa kujumuisha shughuli mbalimbali, ikiwemo upandaji miti katika eneo la bonde la mto Mara, maonesho ya bidhaa za ufundi, michezo, na mijadala ya kitaalamu juu ya uhifadhi wa bonde la mto mara na mazingira kwa ujumla.
Maadhimisho ya Mara Day huadhimishwa kila ifikapo September 15 ya kila mwaka kwa kupokezana kati ya nchi za Tanzania na Kenya, zikiwa ni nchi zenye Bonde la Mto Mara na kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu katika uhifadhi wa mazingira.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti