Taasisi ya Human Brigde iliyoko nchini Sweden kupitia mwakilishi wao nchini Bwana Bahati Kittoh jana Juni 21, 2018 wametoa msaada wa vifaa mbali mbali vya hospitali kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya Shilingi milioni mia nne za Kitanzania viliwasili wilayani Serengeti kwenye kontena lenye urefu wa futi 40 vimetolewa kwa hospitali ya Wilaya inayotarajiwa kuanza kutoa huduma za afya karibuni.
Akiongea kwa niaba ya Human Bridge, Bwana Kittoh anasema kutokana na uongozi mzuri uliopo sasa, taasisi hiyo ikaona haja ya kuunga mkono. “Taasisi hii hutoa misaada kwenye mashirika ya dini, lakini wameshawishika kutoa msaada huu kutokana na uwajibikaji wa serikali” anasema Bwana Kittoh na kuendelea kusema kuwa Taasisi hiyo imekwishatoa misaada kwa Wilaya ya Mkalama na sasa ni zamu ya Wilaya ya Serengeti.
Akipokea msaada wa vifaa hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mheshimiwa Juma Porini anasema huu ni msaada mkubwa kwa wananchi wa Serengeti katika kipindi hiki ambacho Halmashauri inajenga hospitali ya Wilaya huku akiwahakikishia wafadhili wa msaada huo kuwa vifaa hivyo vitatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Tulikuwa na uhitaji wa vifaa hivi katika vituo vya afya pamoja na hospitali ya Wilaya ili kutoa huduma bora za afya kwa wananchi” anasema Mheshimiwa Porini na kuendelea kuchangia “Kwa msaada huu sasa tunaenda kuongeza ubora wa huduma za afya kwa wananchi katika Hospitali ya Wilaya pamoja na Vituo vyetu vya afya.
Aidha Mheshimiwa Porini amewaomba wadau wengine wa ndani na nje ya Tanzania kuchangia katika Sekta ya afya wilayani humo na kuipongeza Taasisi ya Human Bridge kwa msaada huo mkubwa huku akiiomba taasisi hiyo kufika na Sehemu nyingine nchini zenye uhitaji wa msaada huo.
MATUKIO KATIKA PICHA
Mwenyekiti wa Halmashauri, Mheshimiwa Juma Porini (kushoto) akifungua kontena lenye vifaa vya hospitali.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti