Katika juhudi za kuimarisha sekta ya elimu nchini, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kupitia Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeendesha mafunzo elekezi kwa walimu wapya 89 wa shule za msingi na Sekondari mafunzo ambayo yamelenga kuwajengea uwezo walimu hao kuhusu maadili ya utumishi wa umma na haki zao kama watumishi wa serikali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Leo Julai 9,2025 Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti Ndg. Milama Masiko amewahimiza walimu hao kuzingatia maadili ya kazi, kuwa waadilifu, na kuwajibika katika majukumu yao ya kila siku huku akisistiza umuhimu wa walimu kuwa mfano bora kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Mafunzo hayo yamejumuisha mada mbalimbali zinazohusu sheria na kanuni za utumishi wa umma, mbinu bora za ufundishaji, na usimamizi wa rasilimali za shule.
Kwa upande wao walimu wapya walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo, wakisema yamewapa mwanga kuhusu majukumu yao na jinsi ya kuyatekeleza kwa ufanisi huku wakialiahidi kutumia maarifa waliyopata kuboresha kiwango cha elimu katika shule zao na kuchangia maendeleo ya sekta ya elimu nchini.
Mafunzo haya ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuhakikisha kuwa walimu wapya wanaingia kazini wakiwa na uelewa wa kutosha kuhusu majukumu yao na jinsi ya kuyatekeleza kwa kuzingatia sheria, kanuni, na maadili ya utumishi wa umma.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti