Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti limemchagua Diwani wa Kata ya Busawe, Mhe. Ayubu Mwita Makuruma kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2020 hadi 2025.
Uchaguzi huo wa Mwenyekiti umefanyika Desemba 11, 2020 kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa kupiga kura za ndiyo au Hapana ambapo amepata kura zote 41 za ndiyo za Madiwani wateule 40 na ya Mbunge wa Jimbo la Serengeti
Akizungumza baada ya kuchaguliwa na kuunda kamati za madiwani, Mhe. Ayubu Mwita Makuruma (Mwenyekiti wa Halmashauri) amewashukuru madiwani kwa ushindi huo na kuwaahidi ushirikiano wa hali ya juu katika kushughulikia maendeleo ya wana-Serengeti.
“Nawaomba madiwani wenzangu tufanye kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo kwa wananchi wetu wa Serengeti. Ninawaahidi kuwapa ushirikiano wa juu ili kuhakikisha Serengeti inapata maendeleo”
Makuruma ametumia nafasi hiyo pia kuwataka madiwani wote kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wakiwemo Mkuu wa Wilaya, Mbunge na Mkurugenzi wa Halmashauri katika kuwaondolea wananchi vikwazo vya maendeleo kwa kuimarisha miundo mbinu kama barabara, ujenzi wa vyumba vya madarasa na vituo vya afya.
Katika zoezi hilo pia, Uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri umefanyika ambapo diwani wa Kata ya Kisangura, Mhe. Samson Ryoba Wambura (anayeongea - habari katika picha hapo chini) amechaguliwa kwa kupata kura zote 41 za ndiyo
(Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Serengeti Mhe. Samson Ryoba Wambura (Anayeongea hapo juu katika picha)
Mbunge wa Serengeti, Amsabi Mrimi , alipopata nafasi ya kuzungumza amesisitiza vipaumbele vitano vya kusaidia kuinua maendeleo ya Wilaya ya Serengeti
Amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni elimu na afya, utawala bora, mazingira na utalii, Miundo mbinu na uchumi. Amesisitiza kwa kusema kuwa Wanaserengeti tukishirikiana kwa pamoja tunaweza kuiboresha Serengeti na kuifanya jinsi tunavyotaka sisi kwa kusimamia hivyo vipaumbele vitano.
Mbunge wa Serengeti, Amsabi Mrimi (aliyesimama) akizungumza katika kikao hicho
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti