MRATIBU wa TASAF katika Halmshauri ya Wilaya ya Serengeti, Bi. Antusa Swai, amewataka Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia TASAF kutumia fursa hiyo kwa ukamilifu kwa kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza azma ya serikali ya kupambana na umaskini nchini.
Hayo ameyasema jana Mei 19, 2020 wakati wa ziara aliyoifanya katika Kijiji cha Kenyana kilichopo katika Kata ya Ring’wani ya kukagua zoezi la utolewaji wa fedha kwa walengwa hao. Zoezi lililoanza tarehe 13/05/2020 hadi 19/05/2020.
Bi. Antusa akiangalia zoezi la ugawaji wa ruzuku za Mradi wa TASAF katika Kijiji cha Musati Kilichopo katika Kata ya kebanchabancha
Amesema, Walengwa wa TASAF kutobweteka na mafanikio waliyoanza kuyapata kutokana na huduma zinazotolewa na Serikali kupitia TASAF badala yake waendelee kuuchukia umaskini kwa vitendo kwa kufanya kazi kwa bidii ili hatimaye waweze kuboresha maisha yao huku akisisitiza ustawi wa jamii kwa ujumla hususani watoto kama ilivyo dhamira ya Serikali.
Bi. Antusa mesema Serikali hii ya Awamu ya Tano inafanya juhudi kubwa za kuweka mazingira mazuri kwa Wananchi kujiletea maendeleo na kuboresha maisha yao hivyo akawataka kutumia vizuri fursa hiyo kwa kufanya kazi za uzalishaji mali kwa bidii ili kukuza uchumi wao na hatimaye kuchangia katika pato la taifa na kuondoa kero ya umaskini miongoni mwao kwa vitendo.
Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti imepokea shilingi milioni 125,692,000 ikiwa ni fedha kutoka kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) na hii ni kwa mara ya kwanza kwa mwaka huu tangu zoezi hili lilipositishwa kwa muda Machi 2019.
Bi. antusa alisisitiza kuwa fedha hizo hutolewa kwa ajili ya kuboresha maisha ya kaya hizo hasa upande wa elimu, afya pamoja na lishe, ambapo walengwa wanapopata fedha hulenga katika kuinua na kuimarisha familia zilizoko katika mazingira magumu.
Kwa upande wao, wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini , wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais Magufuli huku wakikiri kuwa mpango huo umekuwa mkombozi mkubwa kwao kwani umeweza kuwabadilisha kimaisha na kuiomba serikali kuongeza kiwango cha ruzuku ili kilingane na thamani halisi ya fedha kwa sasa.
Zoezi hili la malipo ya TASAF kwa ajili ya walengwa wa kaya maskini linajumuisha jumla ya vijiji 57 viliyopo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti huku ikilenga kuboresha huduma ya afya, elimu pamoja na upande wa lishe kwa wanufaika wake.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti