“Singita Grumeti Fund ina matumaini kuwa madarasa haya yatatunzwa vizuri ili kusaidia kupata Elimu bora kwa wanafunzi wengi na kuongeza ufaulu wa wanafunzi mbalimbali watakaopata nafasi ya kujiunga na msamo katika shule ya Sekondari Makundusi”
Hayo yalikuwa ni maneno ya Bi. Bahati S. Sumuni wakati wa halfa fupi ya makabidhiano wa Mradi wa Ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Makundusi iliyopo katika kata ya Natta leo tarehe 28 Disemba 2018.
Bi. Bahati aliyekuwepo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Singita alieleza kuwa mradi huu wa ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya sekondari Makundusi ni miongoni mwa miradi mingi ya jamii inayofadhiliwa na kampuni ya Singita Grumeti Fund.
Mradi wa vyumba viwili vya madarasa uliofadhiliwa na kampuni ya Singita Grumeti Fund
Mradi huu umeanza kutekelezwa tarehe 11 Julai 2018 na kukamilika tarehe 11 Octoba 2018 na Singita Grumeti Fund ina mategemeo makubwa kwa uongozi wa shule, wanafunzi na jamii kwa ujumla kuwa watatunza madarasa haya ili yaweze kutumika kwa muda mrefu na kusaidia upatikanaji wa Elimu bora kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Jumla ya gharama iliyotumika kujenga madarasa haya mawili pamoja na kutandaza nyaya za umeme ni shilingi za kitanzania 63,566,401/- (Milioni sitini na tatu laki tano sitini na sita elfu mia nne na moja tu) Kodi ya ongezeko la thamani (VAT) imejumlishwa. Gharama yote ya mradi imefadhiliwa na kampuni ya Singita Grumeti Fund kwa asilimia mia moja.
Naye Diwani wa Kata ya Natta Mh. Juma Porini Keya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ameeleza kwamba anaishukuru Kampuni kwa msaada wanaotoa kwa jamii na Halmashauri ya Wilaya Serengeti kwa ujumla na anaamini kama zipo kampuni, ama watu au mashirika yaliyopata kushuhudia yale yaliyofanya na kampuni hii basi wameshapata kujifunza na yamkini wameshaanza kutekeleza kwingine.
Pia amewaomba walimu kuifanya shule kuwa mfano siyo tu kwa majengo isipokuwa kwa ufaulu wa wanafunzi na ndio itakuwa zawadi ya jamii ambayo badala ya hizo fedha kujigawia kama mikopo ya jamii ikaelekeza kuandaa miundombinu mizuri kwa ajili ya kizazi cha kwao na walimu walipangwa. Aidha ameagiza kuwa miundombinu ya shule itunzwe na ni marufuku kwa yeyote kwa kuingiza mifugo katika eneo la shule.
Mhandisi Juma Hamsini (kushoto) akipokea taarifa ya mradi wa Ujenzi wa madara mawili katika shule ya Sekondari Makundusi.
Mhandisi Juma Hamsini (kushoto) na Mheshimiwa Juma porini Keya (kulia) wakikata Utepe ikiwa ishara ya kufungua rasmi madarasa hayo.
Akipokea Mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mhandisi Juma Hamsini amesema, “Anaishukuru sana Kampuni ya Singita Grumeti Fund na anategemea kuwa kwa ufadhili huu itakuwa chachu kwa wawekezaji na wadau wengine kuja kuwekeza kwenye huduma za kijamii kama hizi”.
Vile vile ameiomba Kampuni hii iweze kuangalia na shule zilizopo pembezoni mwa wilaya kama shule za Busawe na Kisaka na zile zilizopo karibu na Halmashauri ya Bunda kwani nazo zina uhaba wa vyumba vya madarasa. Aidha Mhandisi Juma amemwagiza Mtendaji wa Kijiji Kuona namna bora ya upatikanaji wa madawati katika madarasa hayo.
Na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bw. Peteris Luhunga amesema kuwa, “madarasa hayo yamepunguza changamoto ya madarasa kwa asilimia mia kwani kwa sasa shule iyo ina kidato cha kwanza na cha pili tu na kwa mwakani wanatarajia kupokea wanafunzi mia na sitini tu”.
Aidha amesema, “changamoto kubwa inayowakabili sasa ni Huduma ya umeme na Maji tu japo Shirika la AMREF limewaahidi kuwavutia maji kutoka katika kisima kilichopo jirani”.
Naye Bi. Rhobi ambaye ni mjumbe wa Halmashauri ya Serikali ya kijiji cha Makundusi amesema. “tunaomba Grumeti watusaidie madawati mana mradi tumepokea lakini madawati hakuna na sisi kama Serikali ya kijiji tutaangalia namna ya kuchangia upatikanaji wa madawati hayo”.
Mheshimiwa Juma porini Keya (kushoto), Mhandisi Juma Hamsini (katikati) na Bi. Bahati S. Sumuni (kulia) wakiweka saini katika hati ya makabidhiano ya Mradi wa ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Makundusi. Mradi uliofadhiliwa na kampuni ya Singita Grumeti Fund
Picha ya pamoja kati ya Uongozi wa Kampuni ya Singita Grumeti Fund, Serikali ya kijiji cha Makundusi, Uongozi wa shule na Mkurugenzi Mtendaji (W)
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti