Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ikishirikiana na wadau wake Shirika la Hifadhi ya Serengeti (SENAPA) pamoja na Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) imeanza kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ya Vijiji vya Wilaya ya Serengeti kupitia ufadhili wa Benki ya Wananchi ya Ujerumani (KfW).
“Mpango wa matumizi bora ya ardhi ni endelevu na muhimu kwa kizazi cha sasa na baadae” alisema Dk. Malogo Kongola ambae ni Mshauri elekezi wa Mradi kutoka FZS katika mkutano wa kutambulisha mradi kwa serikali ya Kijiji cha Singisi kilichopo Kata ya Nagusi.
Akitoa shukrani zake za dhati kwa wahisani kuwezesha kijiji chake kuwa miongoni mwa vijiji vilivyopata mradi huo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Singisi Bw. Giroida Dabdera alisema “Mpango huo utawasaidia wakazi wa kijiji chake kupanga na kutumia vizuri rasilimali zilipo kijijini na kuondoa migogoro iliyopo kati ya wakulima, wafugaji na wadau wengine watumia ardhi” Naye Diwani wa Kata ya Nagusi Mhandisi Dickson Manyeresa ameiasa Serikali ya Kijiji kuhakikisha wanabainisha maeneo yote muhimu kwenye mpango na kutenga matumizi kulingana na mahitaji ya sasa na baadae.
Mpango huo umekuja wakati mwafaka ambapo Rais John Pombe Magufuli akiwa tayari ameiagiza Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020, jumla ya vijiji 7,500 viwe na mpango endelevu wa matumizi bora ya ardhi.
Wilaya ya Serengeti ina jumla ya Vijiji 78 ambapo mpaka sasa ni vijiji vitano pekee vilivyokuwa na mpango endelevu wa matumizi bora ya ardhi, huku vijiji 33 vikitarajiwa kunufaika na ufadhili huo.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti