“Nyinyi vikundi hamsini na tano (55) mmeaminika, mmechujwa na mmeonekana kwamba mmekidhi vigezo ambavyo vimewekwa kwa ajili ya kupewa mikopo”
Hayo ni maneno ya Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mh. Nurdini Babu aliyekuwa mgeni rasmi wakati akifungua mafunzo kwa vikundi kuhusu namna ya kutumia kwa tija mikopo inayotolewa na serikali. Mafunzo yaliyofanyika leo tarehe 10/12/2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri
Babu amesema kuwa mikopo hiyo inayotolewa na serikali kupitia makusanyo ya halmashauri ipo na inawahusu wananchi wote ambao wapo tayari kujiunga kwenye vikundi vya uzalishaji mali pamoja na kukidhi masharti na taratibu za kuweza kupatiwa mkopo.
“Fedha hizi ni kwa mujibu wa sheria, lazima kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri tutenge asilimia kumi (10%) kwa ajili ya vikundi mbalimbali, asilimia nne (4%) Wanawake, asilimia nne (4%) Vijana na asilimia mbili (2%) watu wenye Ulemavu”. Amesisitiza babu.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mh. Juma Porini amesema kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Raisi Dr. John Magufuli imeondoa riba kwa vikundi vyote vinapochukua mkopo kutoka Halmashauri lengo likiwa ni kuwaondolea umasikini watanzania hasa wanawake, vijana na walemavu.
“Hatuchaji riba ya aina yoyote kwa hiyo hakuna hata mmoja asiyependa mkopo ambao hauna riba, kama ambavyo nyie mlipata hii fursa, iwe ni lazima na nyie kurudisha kwa wakati ili na wengine pia wapate hiyo fursa ya kukopa bila riba” Amesema Porini.
Mh. Porini akizungumza jambo
Awali akizungungumza wakati wa kutoa taarifa fupi kwa mgeni rasmi; Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya Bw. Wambura Sunday amesema kuwa mikopo hiyo hutolewa kwa vikundi ambavyo tayari vimeshatembelewa na kufanyiwa tathimini na kuona kuwa wanastahili kupewa mikopo, wanaelekezwa namna ya kufanya marejesho, elimu ya ujasiriamali pamoja na elimu ya kuweka na kukopa, na kwa sasa watatoa jumla ya Tshs. Milioni mia moja na ishirini (120,000,000) kwa vikundi vyote hamsini na tano.
Pia Wambura amewapongeza watumishi wa idara ya maendeleo ya jamii, watendaji kata na viongozi wa serikali za mitaa kwa kushirikiana kwa pamoja kusimamia vikundi na kuhakikisha vile vinavyokidhi vigezo ndivyo vinavyopatiwa mkopo ili viweze kuzalisha na kurejesha mikopo hiyo.
Kwa upande wao wanavikundi waliopata mafunzo hayo kutoka Halmashauri ya wilaya ya Serengeti wameishukuru serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo na hatimaye kuwapa mkopo usiokuwa na riba na kusema kuwa wamefurahishwa na hatua hiyo na kwamba shughuli za vikundi hivyo zitafanyika kwa ufanisi baada ya mkopo huo usiokuwa na riba.
Aidha wameahidi kuirejesha mikopo hiyo mapema ili kuwapa nafasi wananchi wengine waweze kukopa.
Wanavikundi mbalimbali wakisikiliza maelekezo kwa makini
Katika robo hii ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya Vikundi hamsini na tano (55) vinatarajiwa kupewa jumla ya Tshs. Milioni mia moja na ishirini (120,000,000) kutoka katika asilimia 10 ya makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri ikiwa vikundi thelatini vya wanawake (Tshs. Milioni sitini), vikundi kumi na tisa vya vijana (Tshs. Milioni hamsini) na vikundi sita vya watu wenye ulemavu (Tshs. Milioni kumi) vitanufaika na mkopo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ili kuwaongezea wananchi husika uwezo wa kujiongezea kipato na kurejesha fedha hizo bila riba ili ziweze kuwasaidia wengine kuinuka kiuchumi.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti