Jimbo la Serengeti limesisitiza kuwa itashirikisha wadau wote wa uchaguzi hususan Vyama vya Siasa katika kila hatua inayopitia kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao wa Mwaka 2020.
Hayo yamesemwa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Serengeti Mhandisi Juma Hamsini wakati kikao cha pamoja na Vyama vya Siasa kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa lengo la kuwafahamisha maelekezo muhimu ya Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 Mwaka huu ili kujenga misingi ya demokrasia inayolenga kuendesha chaguzi huru, wazi na wa kuaminika.
Kwa mujibu wa wa Msimamizi wa Uchaguzi, Jimbo la Serengeti limewashirikisha Vyama vya Siasa katika katika hatua zote muhimu ikiwa pamoja na kuwapatia vitabu vya rejea ambavyo ni Maelekezo ya vyama vya siasa na Maadili ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2020 ikiwa ni sehemu ya kufanikisha zoezi la Uchaguzi Mkuu.
Mhandisi Juma amesisitiza pia vyama vyote vihakikishe vinafuata Sheria na Kanununi zinazosimamia na kuongoza Uchaguzi na iwapo kutakuwa na malalamiko yoyote ni vyema yakawasilishwa kwa maandishi na siyo kwa mdomo. Aidha amesema kuwa Ofisi za Uchaguzi zitakuwa wazi hadi saa mbili kamili usiku na ameshawaagiza Wasimamizi Wasaidizi ngazi ya Kata kuhakikisha kuwa Ofisi hazifungwi.
Akiwasilisha ratiba fupi ya Uchaguzi Msimamizi Msaidizi ngazi ya Jimbo Wakili Maganiko Msabi amesema kuwa fomu za Uteuzi zitatolewa kuanzia Tarehe 12 hadi 25 Agosti, 2020 na uteuzi utafanyika siku hiyo hiyo ya tarehe 25.08.2020, kampeni zitafanyika kuanzia Tarehe 26 Agosti hadi 27 Oktoba, 2020 na Siku ya kupiga Kura itakuwa ni Tarehe 28 Oktoba, 2020
Vyama vilivyoshiriki katika kikao hiki ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi - CUF na Chama cha ACT Wazalendo. Pia vyama vya siasa vyenye usajili wakudumu ambavyo vipo katika Jimbo hili vinakaribishwa kufika katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi ili viweze kutambuliwa uwepo wao katika Jimbo hili hata kama havina ofisi.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti