Serikali Wilayani Serengeti Mkoa wa Mara imelenga kuimarisha mahusiano yenye tija na hoteli za kitalii zilizopo ndani na nje ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Hayo yamebainika katika ziara iliyofanywa na Kamati ya fedha, uongozi na mipango inayoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mhe. Juma Porini Keya ilipofanya ziara kuzitembelea hoteli za kitalii katika hifadhi ya Serengeti. Katika ziara hiyo iliyogawanyishwa katika makundi 4, jumla ya hoteli 15 za kitalii na ofisi za Shirika la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) zilitembelewa.
“Kwa muda mrefu sasa hoteli nyingi za kitalii katika hifadhi ya taifa ya Serengeti zimekuwa hazilipi tozo stahiki hivyo kupunguza vyanzo vya mapato vya Halmashauri; tukiboresha mahusiano, tutaweza kukusanya vizuri mapato ya serikali” alisema Mhe Porini alipokuwa anazungumza na afisa utalii wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti Bw. Aldo Mgude.
Katika kuweka mikakati ya kudhibiti ukwepaji wa kulipa ushuru, kamati imeliomba Shirika kuandaa kikao na kuwakutanisha kwa pamoja na wamiliki wa hoteli za kitalii ili kuboresha mahusiano na kuweka misingi imara ya usimamiaji wa mapato.
Aidha kamati imebaini kiwango kidogo cha upatikanaji wa ajira kwa wakazi wa Serengeti na kuziomba hoteli na kambi za kitalii ndani na nje ya hifadhi ya Serengeti kutoa ajira kwa wakazi wa Serengeti.
Kamati imezipongeza hoteli za kitalii kwa jitihada kubwa wanazofanya kutangaza utalii katika hifadhi ya Serengeti na kuzisaidia jamii zinazoizunguka hifadhi ya Serengeti kwa kutoa misaada ya kielimu pamoja na ujenzi wa miundombinu.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti