Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu (katikati) akipokea msaada wa vitanda 15 kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Mfuko wa Singita Grumeti Bi. Frida Mollel (kushoto)
Mfuko wa Singita Grumeti leo tarehe 3 mwezi Agosti 2017 umetoa msaada wa vitanda 15 vya deka kwa Shule ya Sekondari Serengeti iliyoko katika Kata ya Uwanja wa ndege Wilayani Serengeti kufuatia tukio la kuungua moto kwa bweni la wanafunzi shuleni hapo mwezi oktoba mwaka jana.
Akitoa msaada huo wa vitanda, Mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii kutoka Mfuko wa Singita Grumeti Bi. Frida Mollel amesema kuwa vitandahivyo 15 vyenye uwezo wa kulaza wanafunzi 30 vimegharimu jumla ya Tshs Milioni 7.3. “Sisi ni wadau wa maendeleo na tumeguswa kutoa msaada huu, na kwa sasa tumeweza kutoa vitanda hivi 15 tunaomba mvipokee” alisema Bi Frida.
Akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu hakusita kuwapongeza Singita Grumeti kwa misaada mbalimbali wanayoitoa katika Wilaya ya Serengeti. “Grumeti ni wadau wa maendeleo, wanatoa misaada ya afya, elimu, maji na miundombinu lakini pia wanafadhili nafasi za masomo na kutoa ajira kwa wazawa” alisema Babu na kuwaomba wasisite kutoa misaada zaidi pindi inapohitajika. Aidha Babu amewaonya wanaume wanaowasumbua wanafunzi wa kike kwa kuwataka kimapenzi huku akisisitiza kuwa adhabu kali itatolewa kwa yeyote atakayehusika na vitendo hivyo.
Aidha Katika kuinua taaluma shuleni hapo, Mbunge wa Jimbo la Serengeti Mheshimiwa Marwa Ryoba ambaye ni Mwalimu amejitolea kufundisha masomo ya Kemia na Bailojia katika kipindi chake cha likizo.
Mbunge wa Jimbo la Serengeti (kushoto) Mhe. Marwa Ryoba, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Bw. Juma Hamsini
Tarehe 26 mwezi Oktoba 2016 moto uliunguza jengo la bweni la wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari Serengeti na kuteketeza mali pamoja na nyaraka za wanafunzi zilizokuwa katika bweni na kuwaacha wakiwa na uhaba wa vitanda, madogoro na vyumba vya kulala. Aidha uongozi wa Halmashauri unaendelea na jitihada za kukabili hali hiyo ambapo mpaka sasa ukarabati wa jengo la bweni unakaribia kukamilika.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti