KAMPUNI ya Grumeti Fund kupitia Idara yake ya Maendeleo ya Jamii imeendelea kutoa semina kwa vijana wakiume na wakike Wilayani Serengeti na Bunda ambapo mpaka sasa imefikia mabinti 9,308 na vijana wa kiume 1,018 kuanzia 2017- 2022.
Katika semina hizo mabinti 9,308 kutoka Sekondari 19 za Wilaya ya Bunda na Serengeti, walipewa taulo za kike za kutumia kwa muda wa mwaka mmoja na miezi sita (reusable pads).
Katika kongamano hilo lilofanyika Mwanzoni Mwa wiki Hii, vijana wa kike wameaswa kujituma na kuepuka vishawishi ili kutimiza ndoto zao na kuwa msaada katika Taifa huku ikitoa taulo za kike 761 zinazoweza kufuliwa na kudumu kwa muda wa mwaka mmoja na nusu kwa wasichana wote 761 waliohudhuria semina hiyo.
Akizungumza na wasichana hao katika kongamano hilo, Mgeni rasmi Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Neema Msuya ameipongeza kampuni ya Grumeti Fund kwa kuona umuhimu wa kufanya makongamo hayo na kuwataka wasichana hao kutekeleza yote waliyojifunza ili kutimiza ndoto zao.
"Nawashukuru sana Grumeti Fund, tunatumaini kwa juhudi za wadau hawa hakutuwa na utoro mashuleni, mimba za utotoni, ndoa za mapema na ukeketaji.
"Nyinyi mpo kwenye safari ya maisha, safari bado ni ndefu mkawe na ujasiri, uthubutu, mjiamini mkawe watu bora" amesema Neema
Aidha, ametoa wito kwa mashirika, kampuni na taasisi nyingine kuiga mfano wa Grumeti Fund katika kuendesha semina na makongamano ya kufundisha vijana wa kiume na wakike katika maeneo mbalimbali ili kuwasaidia katika maisha yao.
"Grumeti Fund, naomba muendelee kuwa chachu ya mabadiliko na maendeleo katika Wilaya yetu ya Serengeti na Taifa kwa ujumla" amesema Neema.
Kongamani hilo limehusisha wasichana kutoka shule za Sekondari Issenye, Nagusi,na Rigicha za wilayani Serengeti.
Aidha, amewataka wasichana hao kujituma kielimu na kiujasiriamali ili kutimiza ndoto zao kwa sababu ya uwepo wa mazingira rafiki na amewasihi kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika maisha yao na kuepuka makundi hatarishi na tamaa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Grumeti Fund, Frida Mollel amewakumbusha wasichana hao kuwa wana haki ya kusema hapana kwa mila na desturi potofu ambazo zinawakandamiza na kuwapotezea fursa mbalimbali za kimaisha ikiwemo masomo.
Ameongeza pia:
‘’Mwanamke au binti unanafasi kubwa sana katika jamii kufanya mabadiliko ya kiuchumi, kielimu, na kisayansi’’
Frida amewasisitiza mabinti kuwa wanaweza kufanya chochote na kuwa mtu yeyote na kutimiza ndoto walizonazo, ikiwa watasimama kidete kusimamia maisha yao na kuacha kukumbatia vitu vinavyokwamisha ndoto zao ikiwemo mimba zisizotarajiwa, makundi rika, utoro, ndoa za utotoni na kupoteza muda kwenye mitandao ya kijamii.
Lakini pia ametoa wito kwa wazazi kuunga mkono juhudi za Serikali off kwa kuchangia katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali yakiwemo madarasa na mabweni ili kuboresha elimu zaidi na kufanya watoto kuwa salama.
Grumeti Fund hualika wadau mbalimbali kutoka katika asasi za kijamii ili kuzungumza na mabinti katika maeneo mbalimbali ya maisha yao wakati wa kongamano.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa Chuo cha Sayansi za afya Kisare, Mwl.Restuda Murutta amewataka wasichana hao kuepuka ndoa za utotoni, mimba zisizotarajiwa na kudumisha usafi haswa kipindi cha hedhi.
‘’Tujifunze kujitunza ili kuepuka mimba za utotoni ili kuepuka madhara yatokanayo na kubeba mimba mapema, lakini pia tukumbuke kuweka mazingira yetu ya choo safi ili tusipate magonjwa.’’alisema Mwl Restuda
Nae, Mkurugenzi wa kituo cha nyumba Salama, Hope for Girls and women in Tanzania, Rhobi Samweli ametoa wito kwa wasichana hao kupinga ukeketaji na kuwa chachu ya mabadiliko kwa kuielimisha jamiii juu ya madhara ya ukeketaji na kutoa taarifa ya vitendo vya ukeketaji,
Kupitia Kongamano hilo Wasichana hao walipata wasaa wakuwasilisha changamoto wanazopitia ikiwa ni pamoja na kutoa maoni yao ya namna changamoto hizo zinavyoweza kutatuliwa. Changamoto hizo ni pamoja na ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia kama ukeketaji, kunyimwa haki ya elimu, vishawishi, mila na desturi potofu na kubaguliwa.
Grumeti Fund imekuwa ikitoa ufadhili wa kimasomo kwa vijana, elimu ya ujasiriamali na mazingira kwa jamii pamoja na uhifadhi wa wananyama pori.
Mwisho.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti