Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kupitia Idara ya Ardhi na Maliasili imepokea msaada wa pikipiki tano (5) pamoja na vifaa vya tehama vyote vyenye thamani ya shilingi 43,521,000/= kutoka Shirika la maendeleo la Ujerumani (GIZ)
Makabidhiano ya pikipiki na vifaa hivyo yamefanyika jana tarehe 29/01/2018 katika ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ambapo Bi Dagmar Wittine (Mshauri wa Maendeleo) kutoka shirika la GIZ alikabidhi rasmi vifaa hivyo vilivyopokelewa na watumishi kwa mikono miwili. Bi. Dagmer hakusita kusisitiza juu ya matumizi bora ya vifaa hivyo na kuwataka watumishi wenye uhaba wa vitendea kazi kutuma maombi ili waone namna ya kuisaidia Halmashauri. Aliendelea kwa kusema “Tulipokea maombi ya kusaidia ununuzi wa pikipiki na vifaa hivi kutoka Idara ya ardhi na maliasili mwaka jana (2017) na leo tuko hapo kwa ajili ya kukabidhi vifaa hivyo”
Kupitia msaada huo kutoka Shirika la GIZ sasa watumishi toka Idara ya Ardhi na Maliasili wanatarajiwa kuboresha zaidi utendaji kazi kwa ufanisi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mheshimiwa Juma Porini amewashukuru GIZ kwa kuendelea kuijengea uwezo Halmashuari na kuwaomba kutosita kutoa misaada zaidi pindi inapohitajika. Mheshimiwa Porini pia alisisitiza juu ya matumizi ya pikipiki na vifaa hivyo ili kuleta tija, kwa kusema “Tunakazi kubwa huko vijijini, hivyo pikipiki hizi zitumike katika kazi ya upimaji wa vijiji 36 na natarajia kuona tunakamilisha kazi hiyo kwa wepesi na ufanisi zaidi”
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mhandisi Dickson Kamazima amesisitiza juu ya matumizi bora ya vifaa hivyo kuleta tija na kuwataka watumiaji wa vifaa hivyo kuvitumia kwa umakini na uangalifu zaidi.
Huu ni mwendelezo wa misaada inayoendelea kutolewa na shirika hilo la GIZ ambapo watumishi kutoka idara mbalimbali katika Halmashauri wametakiwa kuandika maandiko miradi ili kuweza kupata misaada toka GIZ.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mhandisi Dickson Kamazima (kushoto) akipokea hati ya makabidhiano toka kwa Bi Dagmar Wittine (Kulia) Mshauri wa Maendeleo GIZ.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mheshimiwa Juma Porini (Kushoto) akisalimana na Bi Dagmar Wittine.
Vifaa vya tehama walivyopatiwa Idara ya Ardhi na Maliasili.
Bi Dagmar akitoa bahasha zenye funguo za pikipiki kwa Watumishi wa Idara ya Ardhi na Maliasili.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti