ZAIDI YA TSH MILION 800 YATUMIKA KUPIMA NA KUANDAA HATI MILIKI ZA KIMILA SERENGETI
Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Anjelina Mabula ameipongeza Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) kwa kutumia zaidi ya Sh Milioni 800 kwa ajili ya kuandaa Hatimiliki za Kimila kwa vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Akikabidhi hati hizo kwa wananchi wa vijiji vya Nyichoka,Nyanungu na Bokore vilivyoko Wilaya ya Serengeti Waziri amesema, Mpango wa shirika huo unasaidia kuongeza thamani ya ardhi na kutatua migogoro ya ardhi kwa wananchi ambayo huchangia vifo na kujeruhiwa kwa wakulima na wafugaji.
Mabula amevitaka vijiji 7 ambavyo bado vina mgogoro wa wakulima na wafugaji na kusababisha wasipiwe ardhi yao vikae chini na kuelewana ili kupata muafaka utakaowasaidia kupata hati miliki kama ilivyo kwa vijiji vingine.
Mapema Meneja wa Mradi huo wa Frankfurt Masigeri Rurai amesema wameanda Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi kwa Wilaya za Serengeti na Ngorongoro kwa asilimia 99 na vijiji 22 kati ya 29 wamefanikiwa kupata hati miliki za kimila na wametumia sh 400 milioni kwa upimaji na sh 400 kwa ajili ya hatimiliki za kimila.
Amesema, vijiji 7 vilivyosalia bado vina mgogoro na kesi ipo mahakamani na wakipata muafaka wataendelea.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Frankfurt Zoological Society nchini Tanzania Dk Ezekiel Dembe amewataka wananchi hati walizopewa wazitunze kwa kuwa Ardhi ni mali na urithi pekee kwa Watoto, na ameipongeza wilaya hiyo kwa kuwapa ushirikiano uliowezesha kukamilisha mradi huo.
Mkuu wa wilaya ya Serengeti Dkt.Vincent Mashinji ameshukuru shirika la FZS kwa kazi kubwa waliyoifanya, ameagiza waliovamia maeneo ya serikali kuondoka haraka kabla ya hatua za kisheria hazijachukuliwa.
Aidha Gertuda Nyambura na Maria Marwa wanufaika na mradi huo wamelipongeza shirika hilo na Waziri kwa kuwapa hati hizo ambazo zitawasaidia kutafutia fursa mbalimbali za maendeleo.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti