Mkuu wa Wilaya Serengeti Dkt. Vincent Mashinji Leo amefanya ziara katika Kata ya Kiambai ili kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa kata hiyo pamoja na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akiwa katani hapo Dkt. Mashinji ametembelea na kukagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Bokore ambapo amepongeza hatua za ujenzi wa Zahanati hiyo.
Aidha katika Kijiji hicho hicho Dkt. Mashinji ametatua changamoto ya mgogoro wa ardhi baina na serikali ya Kijiji na muwekezaji kwa kuwataka wananchi kufuata Sheria ya ardhi ya mwaka 1999 ili kuondokana na migogoro ya ardhi isiyokuwa ya lazima.
Vilevile Dkt. Mashinji katika Ziara yake katani Kyambahi ametembelea na kukagua ujenzi wa nyumba za walimu katika shule ya sekondari Nyichoka ambapo pia amepongeza hatua za ujenzi wa nyumba hizo na kukabidhi mifuko mia moja ya Simenti kwa serikali ya Kijiji cha Nyichoka iliyotolewa na mdau wa maendeleo Bw. Rhimo Nyansaho
Pia Dkt. Mashinji amemaliza ziara yake katika kata ya Kyambahi kwa kufanya mkutano wa hadhara katika Kijiji Cha Nyanungu ambapo katika Kijiji hicho amemtaka mtendaji wa Kijiji hicho kukusanya michango yote iliyotolewa katika harambee ya ujenzi wa shule ya sekondari ya Nyanungu ili ujenzi huo ukamilike na shule iweze kufunguliwa mwakani.
Aidha katika Kijiji hicho Dkt Mashinji amekabidhi mabati ya ujenzi wa Sekondari ya Nyanungu yaliyotolewa na mdau wa maendeleo Bw. Rhimo Nyansaho.
Ziara ya Mkuu wa Wilaya Serengeti Dkt. Vincent Mashinji katika kata ya Kyambahi ni mwendelezo wa ziara yake katika Kata zote za Wilaya ya Serengeti inayolenga kutatua changamoto za wanaserengeti pamoja na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti