Leo tarehe 25/02/2020 Mamlaka ya mji mdogo Mugumu imezindua baraza lake jipya la wajumbe tangu kukamilika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019. Mkutano huu wa uzinduzi umefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya Serengeti ambapo sambamba na uzinduzi huo kuliambatana na shughuli za uapaji wa viapo kwa wajumbe wa viti maalumu, uchaguzi wa mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo, uundaji wa kamati mbalimbali za kudumu na uchaguaji wa wenyeviti wa kamati hizo pamoja na upokeaji wa taarifa ya utendaji na uwajibikaji wa Mamlaka ya Mji mdogo kwa kipindi cha Julai - Disemba 2019.
Baadhi ya wajumbe wa baraza wakisikiliza mkutano
Katika Uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo, Ndugu Chacha Charles Ally ameibuka mshindi wa kiti cha Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo kwa kura Thelathini na mbili (32) kati ya kura Thelathini na mbili (32) zilizopigwa na wajumbe wa baraza hilo aidha Ndugu Mikadady Idd naye ameibuka mshindi wa kiti cha Makamu Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo kwa kura Thelathini na mbili (32) kati ya kura Thelathini na mbili (32) zilizopigwa na wajumbe wa baraza hilo.
Ndugu Chacha Charles Ally Mwenyekiti Mteule wa Baraza la wajumbe wa Mamlaka ya Mji Mdogo Mugumu mara baada ya kukabidhiwa kiti
Taarifa aliyoiwasilisha msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti Bwana Cosmas Quamara amesema kuwa jumla ya kura 32 zilipigwa toka kwa wajumbe 32 huku kukiwa hakuna kura iliyoharibika kwa nafasi zote mbili
"Ndugu Chacha ameshinda kwa kura zote 32 hivyo namtangaza kuwa Mwenyekiti wa Baraza la wajumbe wa mamlaka ya Mji mdogo wa Mugumu na kwa upande wa nafasi Makamu Mwenyekiti Ndugu Mikadady ameshinda kwa kura zote 32 hivyo namtangaza kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la wajumbe wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mugumu " alisema Ndugu Quamara
Ndugu Mikadady Idd Makamu Mwenyekiti Mteule wa Baraza la wajumbe wa Mamlaka ya Mji Mdogo Mugumu
Wakati huo huo Ndugu Quamara amewapongeza wajumbe wote waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24, 2019 na amewataka kuwa wahakikishe wanawatumikia wananchi wa maeneo yao katika kuleta maendeleo ya wananchi hao.
Aidha Mh. Juma Porini ambaye ni Diwani wa Kata ya Natta na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti akitoa neno la salamu katika mkutano huo amewahasa wajumbe wote waliochaguliwa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa kutoa huduma kwa wananchi bila malipo yoyote na kuunga juhudi za Rais wa Jamhuri wa muungano wa Tanzania Mh. John Pombe Magufuli za kuleta maendeleo kwa wananchi.
Pia Mh. Porini amewataka viongozi hao kuwa mfano wa kuigwa kwa wananchi wanao wahudumia kwa uadilifu na maadili pamoja na ushiriki wa shughuli mbalimbali za kijamii.
Wajumbe wa viti maalumu wakila kiapo cha uadilifu
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Bw. Wambura Sunday amewasihi wateule hao kutobwetaka na ushindi mnono walioupata na badala yake waendelee kufanya kazi kwa bidii ikiwemo usimamiaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti