BARAZA la madiwani wa halmashauri ya Serengeti wamepitisha Rasmu ya mpango wa bajeti ya matengenezo ya barabara ya shilingi zaidi ya bilioni 14.268.
Madiwani hao wamepitisha bajeti hiyo kwenye kikao cha baraza la madiwani la kupitisha bajeti ya TARURA kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo kwa ajili ya matengenezo ya barabara,ujenzi wa madaraja,Makalavati na mitaro ya barabara.
Kaimu Meneja wa wakala wa barabara za mjini na vijijini (TARURA ) Mhandisi Charles Marwa akitoa taarifa ya rasmu ya bajeti hiyo alisema katika ukarabati wa barabara na usimamizi zitatumika shilingi milioni 835.7, maendeleo kutoka mfuko wa barabara bilioni 8.183, maendeleo ya bajeti (fedha za jimbo) milioni 500,fedha za maendeleo kutokana na tozo ya mafuta milioni 1 na fedha za maombi maalum kwa ajili ya miradi iliyofanyiwa usanifu kwa madaraja saba na km 2.7za lami kwa shilingi 3.750 bilioni.
Mhandisi Marwa alisema miongoni mwao changamoto ambazoTARURA wanakutanazo wakati wa utekelezaji wa miradi ni pamoja na uharibifu wa miundombinu ya barabara kwa baadhi ya maeneo kutokana na shughuli za binadamu hasa kilimo, ufugaji na mahitaji halisi ya kazi ikilinganishwa na ukomo wa bajeti ya inayotolewa kutoendana.
Nyingine ni pamoja na kutokuwa na ofisi hali inayopelekea kuendelea kupanga kwenye jengo la mtu binafsi , upungufu wa vitendea kazi ,mvua zinazonyesha misimu miwili kwa mwaka zinasababisha kufanya uharibifu wa miundombinu ya barabara mara kwa mara na magari makubwa yenye uzito wa zaidi ya tani 10 yanayopita kwenye barabara.
Amesema hatua walizochukua kuhakikisha wanatatua changamoto hizo watajenga mitaro ya maji, kuweka vigingi vya kulinda eneo la hifadhi ya barabara na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kulinda barabara na kutoa elimu ya katazo la sheria ya barabara na kuchukua hatua kwa kuwakamata magari yanayokiuka sheria hiyo ambapo ameviomba vyombo vya dola viwasaidie pindi watakapohitaji ushirikiano wao.
Licha ya madiwani hao kupitisha bajeti hiyo walisema katika bajeti ya mwaka 22/23 baadhi ya barabara nyingine katika maeneo ya kata zao sio nzuri na kumuomba Mhandisi Marwa aweze kuwafikia na kuweza kuziingiza kwenye mpango wa matengenezo ya barabara.
Diwani wa kata ya Manchira Joseph Kitanana amemuomba pia Mbunge wa jimbo la Serengeti Amsabi Mrimi kwenda kulipeleka suala hilo la bajeti kwani wamekuwa wakipitisha bajeti mara kadha lakini wanaletewa fedha pungufu hali inayopelekea miradi mingi kutofikiwa kwa wakati.
Mbunge Mrimi amewashauri kuingiza baadhi ya barabara katika Wakala wa barabara Mkoa(TANROADS) ambapo ametolea mfano barabara za Tabora B-Burunga na Kenyana B -Gantamome na kumuomba Mhandisi Marwa kuweza kushirikiana nae ili kufanikisha jambo hilo.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti