Aprili 19, 2018 wakazi wa Kijiji cha Ring’wani wanaanza kupata nuru kuona zahanati waliyoanza kujenga ikiwa mbioni kupata ufadhili wa ujenzi kutoka ubalozi wa Japan.
Licha ya kuwa na miaka 31 tangu kuanzishwa kwa Kijiji cha Ring’wani huduma za afya bado ni changamoto kubwa kwa wakazi wa Kijiji hicho. Kijiji hicho kilichopo katika Kata ya Ring’wani Wilaya ya Serenegti hakina zahanati tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1987.
Bi. Sayuri Kon ambaye ni Afisa miradi kutoka ubalozi wa Japan anafika kijijini hapo kujionea hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Ring’wani.
Jengo la zahanati ya Kijiji cha Ring'wani
Ugeni wa Bi. Sayuri kijijini hapo ni matokeo chanya ya andiko mradi lililoibuliwa na mdau wa maendeleo (jina linahifadhiwa) akishirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambapo waliandika andiko hilo kuomba ufadhili wa ukamilishaji wa zahanati hiyo pamoja na nyumba za watumishi kwenda Ubalozi wa Japan.
Bi Sayuri anasema kuwa “tulipokea andiko mradi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti wakiomba msaada wa ukamilishaji wa zahanati, hivyo nimefika hapa kukagua hatua ya ujenzi iliyofikiwa na kuona ni jinsi gani Ubalozi wa Japan utaweza kusaidia kukamilisha ujenzi wa zahanati hii”
Bi. Sayuri Kon (kushoto) akisiliza jambo kutoka kwa wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mhandisi Juma Hamsini anasema kuwa ujio wa afisa huyo kutoka Ubalozi wa Japan ni hatua nzuri ikiashiria uwezekano wa kupata msaada kukamilisha ujenzi.
Naye Diwani wa Kata ya Ring’wani Mheshimiwa Pasto Maiso alimhakikishia Bi. Sayuri kuwa wananchi wapo tayari kutoa ushirikiano ili kukamilisha ujenzi huo huku akimweleza kuwa huduma za maji na umeme zipo jirani hivyo mazingira ya zahanati hiyo yapo vizuri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mhandisi Juma Hamsini (kushoto) akimwonyesha Bi. Sayuri Kon ramani ya jengo la zanahati ya Ring'wani.
Wakazi wa Kijiji cha Ring’wani hutumia saa 2 mpaka 3 kufuata huduma za afya katika Vijiji jirani vya Masiki na Kemugesi. Bi Mgesi Sangi, mkazi wa Kijiji cha Ringw’ani anasema kuwa yeye hutembea kwa masaa 2 kwenda Kijiji jirani cha Masinki kupata huduma za matibabu katika Zahanati huku Bwana Saligoko Rohuro akisema yeye hutumia takribani saa moja na nusu kutembea umbali wa kilomita 8 kwenda Kijiji jirani cha Kemugesi kupata huduma za afya.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ring’wani Bi. Nelimi Masota anasema kuwa kutokana na ukosefu wa zahanati katika Kijiji hicho chenye wakazi wapatao 1930, jamii ilihamasika kujenga zahanati kwa nguvu zao wenyewe na kuchanga shilingi milioni 4. Bwana Juma Patrice, mkazi wa Kijiji cha Ring’wani anasema kuwa kupitia vikao vya kijijini hapo aliguswa kuchangia ujenzi wa zahanati hiyo huku kila kaya ilipaswa kuchangia kiasi cha shilingi 16,500 fedha ambayo anasema amekwisha changa.
Jitihada za wananchi kujenga zahanati zilionekana ngazi ya Wilaya, ambapo Halmashauri pamoja na wadau wengine wa maendeleo waliguswa kuchangia ujenzi wa zahanati hiyo ambayo mpaka sasa imegharimu kiasi cha shilingi milioni 16 na ujenzi umefika hatua ya boma.
Ukosefu wa huduma za afya kwa ngazi za Vijiji (Zahanati) bado ni changamoto kwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, takwimu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu Wilaya ya Serengeti zinaonyesha kuwa Wilaya ya Serengeti ina Zahanati 48 ambazo hazikidhi kutoa huduma za afya kwa Vijiji 78 vilivyopo Wilayani humo.
Halmashauri itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Kijiji cha Ringw’ani kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo ili kuhakikisha adha ya wananchi kutembea umbali mrefu pamoja na vifo vya mara kwa mara hasa kwa mama na moto kukosa huduma za afya zinatatuliwa.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti