Shule ya Sekondari Natta imefanya mahafali yake ya 11 ya kidato cha sita, ambapo jumla ya wanafunzi 111 wamehitimu masomo yao.
Akizungumza na wahitimu wakati wa mahafali hayo Mgeni rasmi Mhe.Amsab Mrimi (Mbunge wa Jimbo la Serengeti) amewapongeza wahitimu na walimu kwa juhudi kubwa walizofanya hadi kufikia hatua hiyo. Aidha, amewakumbusha wazazi na walezi wa wanafunzi kuwa na utamaduni wa kutoa motisha ama zawadi kwa walimu ili kuwapongeza na kuwatia moyo katika kazi yao njema ya ufundishaji na malezi kwa vijana wao ili shule ya Natta iendeleze utamaduni wao wa kufanya vizuri zaidi katika taaluma.
''tunapokutana katika sherehe kama hizi wakati mwingine bebeni zawadi kwa ajili kuwapongeza walimu ili wapate motisha ya kufanya vizuri zaidi''amesema Mrimi.
Aidha, Mhe. Amsabi ameupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kufanya vizuri katika utawala na matokeo ya mitihani ya kitaifa ambapo kwa matokeo ya mwaka jana (2022) shule hiyo ilishika nafasi ya kwanza (1) kati ya shule 22 kimkoa na nafasi ya 11 kati ya shule 644 kitaifa.
Pia, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawanunulia vitabu watoto wao na kuwapa muda wa kutosha wa kusoma ili waweze kupata maarifa, ujuzi na wafaulu katika masomo yao. Amewataka wanafunzi hao kumtanguliza Mungu katika masomo na mitihani yao yote.
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo Mr. Mwema M. Warioba, ametoa wito kwa wanafunzi hao katika kuelekea mitihani yao ya mwisho kuzingatia waliyofundishwa na kuelekezwa na walimu wao na kuhakikisha wanajitahidi na kufanya vizuri katika mtihani wao wa mwisho unaotarajiwa kuanza tarehe 02/05/2023 ''Naomba kila mmoja wenu azingatie tuliyowafundisheni na asome kwa bidii na kuhakikisha anafanya vizuri katika mitihani hii ya mwisho kama tulivyokubaliana".
‘’kwa wanafunzi watano watakaopata division one ya point 3 na 4 tutawalipia gharama za hosteli(accomodation)kwa mwaka mmoja kwa kila mmoja akiwa chuoni. Sambamba na motisha hiyo, mimi binafsi nitatoa tiketi moja ya ndege ya kwenda na kurudi (go and return) kwa mwanafunzi aliyekuwa bora katika taaluma kwa kipindi chote BAHATI A. JUMANNE kwenda katika chuo chochote atakachopangiwa hapa nchini'' amesema Mr. Mwema.
Aidha, Mwl. Mwema ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta jumla ya Tsh. 80,000,000/= fedha ambazo zimetumika kuboresha miundombinu katika shule hiyo kwa kujenga madarasa manne kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita na kupunguza mrundikano wa wanafunzi katika vyumba vya madarasa.
Kwa upande wa wahitimu, wao wameushukuru uongozi wa shule kwa namna ilivyowajali katika kuwahudumia na kuwapa elimu bora kwa kipindi chote walichokuwa shuleni na kuahidi kufanya vizuri zaidi katika mitihani yao ya Taifa. Pia wametoa wito kwa serikali kuisaidia shule kwa kujenga uzio katika shule hiyo kutoka na hatari mbalimbali zinazojitokeza mara kadhaa ikiwemo kuvamia na wanyama wakali pamoja na vibaka wanaohatarisha usalama wa wanafunzi na mali za umma.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti