Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambapo imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti (Kibeyo) ambayo bado ujenzi wake unaendelea, ambapo kamati hiyo imeridhishwa na ujenzi wa hospitali hiyo.
Akizungumza katika kikao cha majumuisho, Makamu Mwenyekiti wa LAAC Mhe. Stanslaus Mabula ambaye ameongoza msafara huo, amepongeza Halmashauri ya wilaya ya Serengeti kwa kazi nzuri iliyofanyika katika ujenzi wa Hospitali hiyo.
“Fundi aliyetengeneza milango ya majengo mbalimbali ya hospitali amefanyakazi nzuri sana na hospitali ina mazingira masafi sana yanayostahili pongezi za Kamati” amesema Mhe. Mabula.
Sambamba na hayo Mhe. Mabula ameitaka Halmashauri kuhakikisha inazingatia sheria, kanuni na taratibu za manunuzi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Ndg. Afrah N. Hassan ameeleza kuwa katika kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo, Halmashauri tayari imejibu hoja zote za Mkaguzi Mkuu na kuziwakilisha katika ofisi za CAG Mkoa wa Mara kwa ukaguzi.
Aidha, Akitolea ufafanuzi suala la mapato Ndg. Afraha amesema kuwa mapato ya halmashauri kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2021/2022 halmashauri haikuwa na ukusanyaji mzuri wa mapato baada ya makampuni ya kitalii zaidi ya 200 kufunga biashara zao kutokana na changamoto ya Uviko 19.
Hata hivyo Ndg. Afraha ameihakikishia Kamati hiyo kuwa kwa mwaka 2022/2123 Halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 4.4 sawa na asilimia 114 mapato ya shilingi bilioni 3.9 zilizokuwa zimepangwa katika bajeti ya mwaka huo huku kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri hiyo ikitegemea kukusanya zaidi kutokana na hatua madhubuti zilizowekwa.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti