Leo tarehe 24/07/2019 ofisi ya Afisa Mwandikishaji Jimbo la Serengeti imeendesha mafunzo ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Maafisa Waandikishaji Wasaidizi wa Kata zilizopo katika Jimbo la Serengeti.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ambapo wawezeshaji walikuwa ni Maafisa Waandikishaji Wasaidizi wa Jimbo, Afisa Uchaguzi wa Wilaya na Afisa TEHAMA wa Wilaya
Bw. Nyambita Zakayo (Afisa TEHAMA wa Wilaya) akitoa mafunzo kwa washiriki wa semina (hawapo Pichani
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo Mgeni rasmi ambaye ni Afisa Mwandikisahaji Msaidizi Jimbo, kwa niaba ya Afisa Mwandikishaji Ndg. Victor Rutonesha alisema “Mafunzo haya yatahusisha ujazaji wa fomu zote zitakazotumika katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na mafunzo kwa vitendo yatakayohusu namna ya kutumia mashine za kusajilia (BVR Kits)”
Pia Ndg. Rutonesha ameongezea kwa kusema “mafunzo ya jinsi ya kutumia mfumo wa Uandikishaji yanalenga kuwawezesha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata kupata uelewa wa jinsi ya kutumia kwa ufasaha BVR Kit kwa ajili ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na wao waweze kutoa mafunzo hayo kwa BVR Kit – Opereators na Waandishi Wasaidizi ambao ndio watahusika na uandikishaji wa Wapiga Kura vituoni”
Aidha Ndg. Rutonesha amewataka Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata waliowahi kushiriki zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Miaka iliyopita kutumia uzoefu walioupata kuwasaidia Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata ambao hawakuwahi kushiriki katika mazoezi yaliyokwishapita
“Ni matumaini yangu kuwa, kwa kutumia uzoefu mlionao, mtafanya kazi zenu kwa ufanisi mkubwa, kwa bidi na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hili. Vile vile mtatumia uzoefu wenu mlionao kuwasaidia wenzenu ambao hawakuwahi kushiriki katika zoezi lililopita kutekeleza majukumu yao kikamilifu” alisema Ndg. Rutonesha
Pia Ndg Rutonesha amewakumbusha Maafisa hao kuwa Mawakala wa vyama vya siasa wanaruhusiwa kuwepo katika vituo vya Kuandikishia Wapiga Kura kwa kuwa jambo hilo ni muhimu na linasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima la Uandikishaji. Lakini hawatakiwi kuwaingilia watendaji wanapotekeleza wajibu wao.
Baadhi ya washiriki wa semina wakimsikiliza Mwezeshaji (hayupo pichani)
Na mwisho amewataka Maafisa hao kuwa na ushirikiano na wadau mbali mbali ili kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa ufanisi mkubwa.
“Ni muhimu uwepo ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wote wa zoezi hili, vyama vya siasa na wadau wengine wote. Ninawasihi muwe na ushirikiano mzuri na wa karibu na waandikishaji ngazi ya Jimbo wakati wote mtakapokuwa mnahitaji ufafanuzi au maelekezo katika kazi yenu” alisema Ndg. Rutonesha
Washiriki wa semina wakifuatilia mada
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wamesema kuwa mafunzo haya yatawasaidia katika zoezi zima la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na wanaahidi watafanya kazi hii kwa utiifu na weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa ufanisi mkubwa
Naye Afisa Mwandikishaji Jimbo Mhandisi Juma Hamsini aliwasisitiza Maafisa Waandikishaji Wasaidizi wa ngazi ya Kata kufanya kazi kwa Umakini, ufanisi na kuzingatia viapo walivyopokea katika utendaji wao.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti