Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Dk. Deo Kisaka (kulia) akitoa maelezo ya mchoro sanifu wa hospitali ya Wilaya ya Serengeti kwa Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 06 Juni 2017 amefanya ziara ya kikazi Wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara.
Katika ziara hiyo Makamu wa Rais ametembelea Kijiji cha Kibeyo nje kidogo ya Mji wa Mugumu ambapo ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Serengeti unaendelea na kuweka jiwe la msingi hospitalini hapo na kisha kufanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa mbuzi katika Mji wa Mugumu.
Hafla ya kuweka jiwe la msingi katika hospitali ya Wilaya pamoja na mkutano wa hadhara zilihudhuliwa na umati mkubwa wa watu pamoja na viongozi mbali mbali kutoka mkoa wa mara wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk. Charles Mlingwa.
Taarifa aliyoitoa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu kwa Makamu wa Rais, amebainisha changamoto ya ukosefu wa fedha katika kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo. “Hadi kufika mwaka 2014 jumla ya Tshs 1,859,284,000 zilikwisha tumika katika ujenzi wa hospitali, na kuanzia mwaka 2015 mpaka sasa bado hatujapata fedha kukamilisha ujenzi wa hospitali” alisema Babu. Aidha Mkuu wa Wilaya amesema Jumla ya Tshs 1,478,859,289 zinahitajika katika kukamilisha ujenzi wa majengo ya wagonjwa wa nje (OPD) katika awamu hii ya kwanza ya ujenzi na anatarajia ifikapo mwezi Disemba huduma za afya ziwe zinatolewa.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amepongeza juhudi zilizofanywa na uongozi wa Serikali, viongozi wa siasa pamoja na wadau wa maendeleo ndani ya Wilaya ya Serengeti na Mkoa wa Mara katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya.
“Leo hii tunahimiza ujenzi wa hospitali na vyumba vya upasuaji Tanzania nzima, kweli mmefanya kazi nzuri hospitali haijaisha lakini mpaka mlipofika nimejua hapa watu wako makini. Nawapongeza kwa hatua mliyofikia” amesema Makamu wa Rais. Aidha Mhe. Samia Suluhu ameahidi kuchangia Shilingi Milioni 5 katika ujenzi wa hospitali unaoendelea huku akiahidi kusimamia ujenzi wa hospitali na kuhakikisha serikali inaleta fedha ili kukamilisha ujenzi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Serengeti Mhe. Marwa Ryoba Chacha ameiomba serikali kuleta fedha kwa wakati ili miradi iliyokusudiwa na kuanzishwa iweze kukamilika kwa wakati. “Kukamilika kwa hospitali hii kutasaidia wananchi pamoja na watalii wanaotembelea Hifadhi yaTaifa ya Serengeti kupata huduma bora za afya ndani ya Wilaya ya Serengeti” amesema Mhe Mbunge.
Ujenzi wa hospitali ya Wilaya ulianza mnamo mwaka 2009 kupitia mkandarasi Gross Investment Ltd na kufikia mwaka 2015 ujenzi ulisimama kutokana na ukosefu wa fedha. Ziara hii ya Makamu wa Rais inaleta mwanga wa matumaini ya kukamilika kwa hospitali hiyo ifikapo mwezi Disemba 2017 na wananchi kupata huduma bora za afya ndani ya Wilaya ya Serengeti.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti