Wakati dunia ikiadhimisha siku ya kisukari duniani kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu ongezeko la ugonjwa huo na mikakati ya kuzuia na kudhibiti tishio lake, Hospitali ya Nyerere DDH Serengeti Mkoani Mara, imefanya huduma ya vipimo vya kisukari na shinikizo la damu bure kwa lengo la kuwafanya wananchi kuwa na uelewa mpana juu ya magonjwa hayo na kutambua afya zao.
Dkt. Ediga Saulo ni Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nyerere DDH iliyopo Wilayani Serengeti Mkoani Mara amesema lengo la kutoa huduma hiyo bure kwa wananchi katika siku hii ni kuhakikisha jamii inakuwa na ulewa mpana juu ya kisukari na shinikizo la damu lakini pia ni kuhakikisha watu wanakuwa na tabia ya kupima afya zao mara kwa mara jambo ambalo pia limesisitizwa na shirika la Afya Duniani - WHO.
Dkt. Saulo ameongeza kuwa ili jamii iweze kupambana na kisukari ni lazima kubadili mtindo wa maisha ikiwa ni kupunguza ulaji wa kiasi kikubwa cha vyakula vya wanga na kuepuka ulaji wa chumvi na mafuta uliopitiliza sambamba na kupunguza matumiza ya pombe kupita kiasi.
"moja ya sababu zinazopolekea ongezeko la ugonjwa wa kisukari katika jamii zetu ni ulaji uliopitiliza wa vyakula vya wanga, mafuta na chumvi iliyopitiliza, matumizi ya vyakula hivi huchangia kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa kisukari" alisema Dkt. Saulo
Dkt. Ediga Saulo Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nyerere DDH Serengeti.
Aidha ameongeza ulaji wa mboga mboga na matunda kwa wingi na ufanyaji wa mazoezi pia ni njia nyingine zinazoweza kuinusuru jamii na ugonjwa huu wa kisukari.
Kwa upande wa wananchi wa waliopata huduma ya vipimo bure wameushukuru uongozi wa Hospitali ya Nyerere DDH kwa kulipa kipaumbele suala hili kwani awali iliwawia vigumu kupata huduma ya kupima afya zao kutokana umbali na kukosa fedha za kulipia vipimo hivyo.
Kulingana na takwimu za Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO Watu milioni 24 wanaishi na kisukari barani Afrika na idadi hiyo inatarajiwa kufikia milioni 55 mwaka 2045 endapo juhudi za makusudi hazitachukuliwa.
Siku ya kisukari duniani huadhimishwa kila mwaka Novemba kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu ongezeko la ugonjwa huo na mikakati ya kuzuia na kudhibiti tishio lake.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti