“Zamani nilikuwa katika hali ngumu sana, nilikuwa sina chochote kile. Nawashukuru sana Tasaf kuja na mpango huu, maendeleo niliyonayo sasa ni mazuri”
Hiyo ni kauli ya mnufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini (awamu ya tatu) kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bi. Verediana Sakwe mkazi wa Kijiji cha Makundusi, Kata ya Natta wilayani Serengeti akiongelea manufaa aliyoyapata tangu kuingia kwenye mpango huo.
Bi. Verediana ambaye ni mama wa watoto wanne anasema kuwa kupitia fedha alizokuwa anapata kutoka Tasaf amefanikiwa kuanzisha mradi wa ufugaji kondoo pamoja na biashara ya mahindi. Katika shughuli ya ufugaji alianza na kondoo wawili huku akiishi katika nyumba yake ya awali (nyumba ya tembe) ambayo aliibomoa baada ya kuanza kunufaika na miradi aliyoanzisha.
Bi. Verediana akichunga mifugo yake (kondoo) jirani ya nyumbani kwake, kijijini Makundusi.
“Nilianza kuwa kufuga kondoo wawili huku nikiishi katika nyumba ya tope, niliendelea na hali hiyo mpaka nilipokusanya fedha za kutosha kujenga nyumba yangu hii mpya ta tofali za kuchoma” anasema Bi. Verediana. Huku akiendelea kwa kusema namshukuru mungu kwa sasa naendelea vizuri nina kondoo 20 na naendela na biashara”
Bi. Verediana akitoka kwenye nyumba aliyojenga kutokana na matunda ya fedha za Tasaf.
Naye Bi. Chausiku Tareta mkazi wa kijijini hapo amefurahishwa na mpango huo kutokana na matunda anayoyapata kupitia fedha za Tasaf. “Nilikuwa nafanya biashara ya mbogamboga na kufanikiwa kupata faida ya shilingi elfu kumi ambayo niliitumia kuanzisha biashara ya kuuza supu” Bi. Tareta akielezea hali aliyokuwa nayo kabla ya kuingia kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini. Kupitia fedha za Tasaf Bi. Tareta amekuza biashara yake na sasa ana duka la vitu vya reja reja huku akiishukuru Tasaf kwa kumkwamua katika umasikini.
Licha ya kuanzisha biashara mpya Bi. Tareta bado anaendelea kuuza supu inayopatikana pembeni kidogo ya duka lake “Kwa sasa nauza vitu hapa dukani lakini pia naendela na kazi yangu ya kuuza supu, nawashukuru sana Tasaf kwa kunisaidia”
Bi. Tareta mkazi wa Kijiji cha Makundusi, Kata ya Natta akionyesha biashara ya duka aliloanzisha kutokana na fedha za Tasaf.
Toka kuanza kwa mpango huo Mwezi Julai mwaka 2015 jumla ya shilingi Bilioni 2.6 za kitanzania zimetumika kuwanufaisha walengwa kwa kaya 3,666 za Wilaya ya Serengeti. Aidha kaya 228 zimeondolewa kutokana na sababu za kukosa sifa kuendelea kuwa kwenye mpango na kufanya kaya zilizosalia kwenue mpango kuwa 3,438. Anasema Mratibu wa mpango wa kunusuru kaya masikini awamu ya tatu (3) Bi. Antusa Swai.
Akitaja sababu za kukosa sifa, Mshauri wa mpango huo Bwana Sokoro Munubi amezitaja sababu zinazisababisha wajumbe kukosa sifa ni; wajumbe kuhama makazi walioandikishiwa, kufariki pamoja na wanufaika kutokwenda kuchukua fedha mara tatu mfululizo hivyo kusababisha kuondolewa kwenye mpango.
Licha ya kutolewa kwa fedha hizo kwa kaya masikini ili kuboresha hali za maisha na kuanzisha miradi mbalimbali, bado kuna changamoto ya walengwa kutotumia fedha hizo kwa matumizi yaliyokusudiwa huku baadhi yao wakiwa katika hali zile zile kabla ya kuingia kwenye mpango.
Bi. Antusa Swai anakiri kuwepo kwa changamoto hiyo na ofisi ya Tasaf wilayani kwa kushirikiana na maafisa wa maendeleo ya jamii ngazi ya Kata wamekuwa wakishirikiana katika kutoa elimu ya ujasiliamali ili kaya ziweze kuanzisha miradi itakayowaingizia kipato. “Huwa tunatoa elimu ya ujasiliamali kupitia maafisa ugani waliopo ngazi ya Kata na Vijiji lakini pia wakati wa malipo huwa tunawaelimisha walengwa kuanzisha miradi itakayokuwa inawaingia kipato” anasema Bi. Antusa Swai.
Mpango wa kunusuru kaya masikini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Wilaya ya Serengeti ulianza kuwanufaisha walengwa waliohakikiwa kupitia uchunguzi na uliofanywa na wataalam na kupitishwa na vikao ngazi za vitongoji na vijiji ili kuwabaini walengwa halali waliostahili kupatiwa misaada.
31603 Stendi Kuu | Serengeti
Anuani ya Posta: 176 Mugumu Serengeti
Simu ya mezani: 0282985686
Simu: 0782677763
Barua pepe: ded@serengetidc.go.tz
Hakimiliki © 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti